1. Muogope Mungu bosi, Ramadhani inapita Mda wote simuasi, yupo na atakupata Usije fanya uasi, Yeye yu hai si mata Tumuogop...
1. Muogope Mungu bosi, Ramadhani inapita
Mda wote simuasi, yupo na atakupata
Usije fanya uasi, Yeye yu hai si mata
Tumuogope Mwenyezi, Ramadhani ni mpito.
2. Watu walishika kasi, kutubia kwa matata
Kuachana na visasi, ibada kuzikamata
Ugomvi sisi kwa sisi, kila ovu lilisita
Tumuogope Mwenyezi, Ramadhani ni mapito
3. Mwezi ukaribiapo, watu hutubu kwa hima
Huacha yao michapo, na ibada kusukuma
Ingawa wachache tupo, tusojali ya Karima
Tumuogope Mwenyezi, Ramadhani ni mapito
4. Mungu yupo siku zote, apasa kuabudiwa
kwa lolote kwa chochote, ndie wa kushukuriwa
Usingoje yakupate, au mwezi kufikiwa
Tumuogope Mwenyezi, Ramadhani ni mapito
5. Waliacha kutambika, Kisa mwezi unakuja
Kwa muda wakaongoka, Kutatua zao haja
Mwezi ukisha toweka, wanarudia vioja
Tumuogope Mwenyezi, Ramadhani ni mapito
6. Yule kamwacha Rehema, kwasababu amuiba
Imemjaa heshima, tadhani katoka SOBA
Mwezi ukisha pogoma, wanarudia mahaba
Tumuogope Mwenyezi, Ramadhani ni mapito
7. Kaolewa dada yetu, na yule kijana HAJI
Kasitiri wake utu, Watoto tunataraji
Lakini isiwe tu, kisa apikiwe uji
Tumuogope Mwenyezi, Ramadhani ni mapito
8. Ramadhani mwezi bora, Hilo tusilikatae
Ziwazi zake ishara, Na achume achumae
Tupate njema bishara, Na kwa Mola tutubie
Tumuogope Mwenyezi, Ramadhani ni mapito
9. Mwezi huu kama lulu, na ukweli ndio huo
Lengo waja tufaulu, Ramadhani kama chuo
Kwa kauli na FIILU, tuachane na puuo
Tumuogope Mwenyezi, Ramadhani ni mapito10. Mwezi ukiisha bwana, Usiyaache mazuri
Endeleza, shikamana, Mungu atakupa heri
Tutafuzu kwa Rabana, Tung'aze zetu kaburi
Tumuogope Mwenyezi, Ramadhani ni mapito
Shairi hili limetungwa tar 17.06.2017 saa 10:18 jioni (Ramadhan 22 1438 - Jumamosi)
Saidi R. Bunduki
COMMENTS