Cheka ki star kaka, ndivo yalivo maisha
Kesho utapumzika, pumzi unazishusha
Ukipata cheka cheka, ukikosa wakausha
Maisha safari ndefu, vumilia kibogoyo.
Ulichonacho ridhika, hata ka hakikutosha
Kesho utahangaika, Mungu atakupatisha
Usije ukaropoka, kwamba amekukosesha
Maisha safari ndefu, vumilia kibogoyo.
Hali mbaya umechoka, punguza yako presha
Ipo siku itafika, wahaka ataondosha
Mungu wetu wa Baraka, ndie ano tuendesha
Maisha safari ndefu, vumilia kibogoyo.
Kuna kitu unataka, sasa una mshawasha
Kama mipesa kushika, mambo yako kuendesha
Punguza kuhangaika, miaka haijaisha
Maisha safari ndefu, vumilia kibogoyo.
Fulani kafunga mwaka, gari kwake kaegesha
Mwaka huu amewaka, akija mbali wapisha
Wewe kwako kimenuka, mawazo kucha wakesha
Maisha safari ndefu, vumilia kibogoyo.
Kwa yule yamenyooka, mamboye ana bashasha
anahisi keshafika, hakuna wa kumshusha
mwambie sije ropoka, Mungu ndo amuendesha
Maisha safari ndefu, vumilia kibogoyo.
Imepita mingi myaka, ndoa inakuzungusha
Kwa yule unomtaka, matatizo akuvisha
Tafuta usijechoka, ipo siku yatakwisha
Maisha safari ndefu, vumilia kibogoyo.
Umesoma umechoka, masomo yakuzeesha
Kutwa una chakarika, ajira kujipatisha
Uko hoi nyaka nyaka, bado hujafanikisha
Maisha safari ndefu, vumilia kibogoyo.
Baba mkwe kacharuka, mwenzako kalianzisha
Hujajua pakushika, ndoa inakutingisha
Watamani kuachika, ni nani atakulisha?
Maisha safari ndefu, vumilia kibogoyo.
Dunia ina WAHAKA, nadhani hautobisha
Wengi tuna weweseka, kutwa kutafuta ndisha
Akili zimeturuka, ni nani wakutukosha
Maisha safari ndefu, vumilia kibogoyo
Vumilia dada, kaka, pupa yako pumzisha
Utafute kwa mipaka, Mwenyezi kumridhisha
Tapata unachotaka, Ishallah nakukumbusha
Maisha safari ndefu, vumilia kibogoyo
Fukweni chombo naweka, nchi kavu najishusha
Fukweni chombo naweka, nchi kavu najishusha
Kalamu imedondoka, pia wino umeisha
Pembeni najisopeka, wajuao nawapisha
Tutajakutana tena, Rabi akitujalia.
Karibuwa kwenye blog yangu.
sayyidbunduki.blogspot.com
/ bunnduki.over-blog.com
COMMENTS