Sifa njema zote Anastahiki Allaah Mola wa viumbe vyote na Swalah na salamu zimfikie Mtume wetu na kipenzi chetu Muhammad (Swalla Allaah...
Sifa njema zote Anastahiki Allaah Mola wa viumbe vyote na Swalah na salamu zimfikie Mtume wetu na kipenzi chetu Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) na aali zake na sahaba zake wote.
Ama
kwa hakika katika mwezi wa Ramadhwaan kuna fadhila nyingi ambazo mimi
nitazitaja kwa uchache namuomba Allaah Aniwafiqishe 'asaa yawe na
manufaa katika Duniya na Akhera.
1) NI MWEZI WA QUR-AAN
Kama Alivyosema Allaah Mtukufu:
"Mwezi
wa Ramadhwaan ni mwezi ambao imeteremshwa Qur-aan ili iwe uongozi kwa
watu na hoja na upambanuzi (Baina ya haki na batil)” [Qur-aan 2:185]
Vilevile
kama ilivyopokewa na Ibn 'Abbaas (radhiya Allaahu 'anhu) kuwa
makusudiyo yake kwa hakika kuteremshiwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi
wa sallam) Qur-aan mwanzo ni katika mwezi wa Ramadhwaan na vilevile
Qur-aan mwanzo wa kuteremka ni usiku wa Laylatul-Qadir na Laylatul-Qadir
iko katika mwezi wa Ramadhwaan.
Hivyo basi ni juu yetu kufanya juhudi katika mwezi huu kukithirisha sana
kusoma Qur-aan. Walikua Salafus-Swaalih (Wema Waliotangulia)
wakikilinda kitabu cha Allaah kwa kukisoma na kuyafanyia kazi
yaliyokuwemo kwa mazingatiyo. Pia Tunaambiwa kuwa Sayyidnaa Jibriyl
(‘Alayhis-Salaam) akimfundisha Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam)
Qur-aan katika mwezi wa Ramadhwaan, na alikuwa 'Uthmaan bin 'Afaan
(Radhiya Allaahu 'anhu) kila siku akisoma Qur-aan yote yaani
anakhitimisha mara moja kwa siku, kwa maana, msahafu mzima anausoma
kwa siku moja. Na walikuwa baadhi yao
katika wema wakisoma Qur-aan yote kwa siku tatu, wengine kwa wiki moja
na wengine kwa siku kumi. Walikuwa wakisoma Qur-aan ndani ya Swalah na
nje ya Swalah.
Allaah Atuwafiqishe mimi na wewe tuisome Qur-aan na kwa mazingatio khasa katika mwezi huu tufanye juhudi sana ili tuweze kupata fadhila za mwezi huu mtukufu.
2) NI MWEZI WA SUBIRA
Subira
ni katika jambo gumu na halipati ila kwa mtu mchaji Allaah na
mnyenyekevu kwa Allaah. Na katika kufunga kunatakiwa subira pale mtu
anapojizuilia kutokana na kutokula, kunywa, matamanio na mengineyo.
Imekua Swawm ni nusu ya subira na subira malipo yake ni pepo kama alivyosema Allaah Mtukufu:
"Kwa hakika (Allaah) Atawapa wenye kusubiri malipo bila ya hisabu" [Qur-aan 39:10]
3) MILANGO YA MOTO INAFUNGWA, MILANGO YA PEPO INAFUNGULIWA NA MASHETANI WANAFUNGWA
Kama ilivyokuja katika Hadiyth iliyopokelewa na Maimamu wawili:
Mtume
(Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) amesema, "Pindi inapokuja Ramadhwaan
inafunguliwa milango ya pepo, na hufungwa milango ya moto, na mashetani
wanafungwa kwa Minyororo." [mesimuliwa na Al-Bukhaariy na Muslim]
Kwa hakika utaona
katika mwezi huu watu wengi wanajitahidi kujiepusha na maasi, watu
wanajaa misikitini kwa kufanya ibada ya mwezi huu hii ni kwa sababu
mashetani wamefungwa na shetani juu ya uasi wake lakini anauogopa mwezi
wa Ramadhwaan na vitimbi vyake vinakuwa dhaifu ndio mana wengi nyoyo
zinabadilika wanaswali na kujitahidi kufanya kheri. Lakini ikimalizika
Ramadhwaan tu basi Swalah imekwisha kama vile Allaah yupo Ramadhwaan tu. Huu ni msiba ndugu zangu Waislamu Allaah Asitujaalie katika hao.
4) LAYLATUL QADR
Katika mwezi huu kuna siku ya Laylatul-Qadr siku ambayo ni bora kuliko miezi elfu kama Alivyosema Allaah:
"Huo ni usiku wa hishima ni bora kuliko miezi elfu.
Huteremka Malaika na roho (za viumbe watakatifu) katika (usiku) huo
kwa idhini ya Mola kwa kila jambo.
Ni amani (usiku) huo mpaka mapambazuko ya alfajiri"
[Qur-aan 97:3-5]
Imehisabiwa mtu atakapofanya ibada katika usiku huo mmoja ni kama amefanya ibada sawa na miaka 83 na hii ni katika fadhila kubwa kabisa. Na katika kitabu Muwatwaa, Imamu Maalik amesema.
Mtume
(Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) ameona umri wa ummah za mwanzo ni
mrefu, na umri wa ummah wake ni mfupi akapewa usiku wa Laylatul-Qadr uwe ni bora kuliko miezi elfu.
[Muwatwaa, 1/321]
Hakuna siku tukufu na kubwa kama
siku hii ni wajibu kwetu kuutafuta usiku huu katika kumi la mwisho
kufanya ibada ili tupate fadhila hizo. Ninamuomba Allaah atuwezeshe kwa hilo, Aamiyn.
5) DU'AA NI ZENYE KUKUBALIWA
Katika hadiyth iliyopokewa na Imaam Ahmad:
Kutoka kwa Jaabir (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwa isnadi iliyo nzuri
Mtume
(Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) Amesema: "Kila Muislam du'aa zake ni
zenye kukubaliwa atapomuomba katika mwezi wa Ramadhwaan"
Na
imepokewa katika Hadiyth kuwa du'aa ya mwenye kufunga pia ni yenye
kukubaliwa. Basi mtu ajipinde katika kumuelekea Allaah kumuomba mambo ya
kheri ya dunia na akhera aombe pepo ya Jannaatul Firdaus na alete
maombi mengine, Allaah Atayapokea maombi yetu, AAMIYN.
La mwisho ambalo nitakua nimekamilisha maudhui yangu:
6) MWEZI HUU NI MWEZI WA KUTOA
Na alikua Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) akizidisha kheri nyingi katika mwezi wa Ramadhwaan.
Imepokewa na At-Tirmidhiy kutoka kwa Anas (Radhiya Allaahu 'anhu) Kasema Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) "Bora ya (wakati wa) kutoa sadaqa ni kutoa katika mwezi wa Ramadhwaa.n"
Na
imepokewa na Zayd bin Aslam kutoka kwa babake, amesema nimemsikia 'Umar
bin Al-Khattwaab (Radhiya Allaahu 'anhu) anasema, "Ametuamrisha Mtume
(Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) tutoe sadaqa nikatoa mali yangu nikasema leo nimemtangulia Abu Bakr nimekwenda na nusu ya mali, akasema Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) kuniambia, "Umewabakishia nini watu wako?" Nikasema, nusu kama hii, na akaja Abu Bakr na kila mali
yake Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) akamuuliza,
"Umewabakishia nini watu wako? Akasema, nimewabakishia Allaah na Mtume
wake. Nikasema huyu Abu Bakr hapitiki na kitu chochote abadan"
Kuonyesha
wema waliotangulia walikua wakishindana katika kheri lakini tofauti
kubwa katika zama zetu hizi watu wanashindana katika mambo ya kidunia na
kujifakharisha nayo.
Tunamuomba
Allaah Atuonyeshe mema tuyafuate na mabaya tuyawache na tushindane
katika kila kheri ili tuwe ni wenye kufuzu na kupata daraja ya juu ya
Pepo.
COMMENTS