FAMILIA NA MWEZI WA RAMADHANI

 TUNAKUMBUSHANA MAMBO YA FAMILIA KATIKA MWEZI WA RAMADHANI. Shukrani zote ni za Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Ni katika baraka zake...

 TUNAKUMBUSHANA MAMBO YA FAMILIA KATIKA MWEZI WA RAMADHANI.


Shukrani zote ni za Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala)
Ni katika baraka zake Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) kwa Muislamu Kumuwezesha kufunga mwezi wa Ramadhani na kuutumia wakati wake wa usiku kwa Swalah. Ni mwezi ambao ndani yake amali njema huzidishwa malipo  na watu hupandishwa daraja (vyeo). Ni wakati ambao Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Huwaachia huru baadhi ya watu kutokana na Moto. Kwa hivyo Muislamu ni lazima ajitahidi sana kufanya mambo mema katika mwezi huu; ni lazima afanye hima katika kuutumia wakati wa uhai wake wenye ibada. Kuna watu wangapi ambao wamenyimika katika mwezi huu kutokana na maradhi, mauti au kukosa maelekezo mema.

Muislamu ni lazima ajitahidi sana (kufanya matendo mema) katika wakati wake wote ndani ya mwezi huu; anayo majukumu yasiyoweza kuepukika juu ya watoto wake, kuwalea  vizuri na kuwatunza vyema,  kuwahimiza kufanya kila aina ya vitendo vyema na kuwafanya waendelee kukuwa navyo – kwa sababu  mtoto hukulia katika mwenendo ambao wazazi wake wamemzoeza.
  
Katika wakati wa siku hizi zilizobarikiwa, baba na mama wana nafasi adhimu ya kufanya yenye manufaa, na tunaweza kutoa ushauri ufuatao kwa wazazi:

1 - Kuzifuatilia Swawm za watoto wao na kuwapa moyo wale  wanaoshindwa kufanikisha.

2 - Kuwahimiza kuhusu  Swawm halisi inavyotakiwa, na sio tu kujizuilia kula na kunywa, lakini ni njia ya kufikia kwenye Kumcha Allaah (Taqwa), na hiyo ni nafasi maalumu ya kusamehewa madhambi na kulipwa malipo mema.

Imesimuliwa kutokana na Abu Hurayrah kwamba Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alishuka kutoka juu ya minbar na akasema : “Aamiyn, Aamiyn, Aamiyn.” Akaulizwa, “Ewe Mjumbe wa Allaah, kwa nini umefanya hivyo?” Akasema, “Jibriil alinambia, ‘amekula khasara yule ambaye Ramadhwaan imemfikia na akawa hakusamehewa dhambi zake, na nikasema , ‘Aamiyn’. Baadaye akasema, ‘amekula khasara yule ambaye ameishi na hali ya kuwa amewaona wazazi wake mpaka wakawa vizee, mmoja wao au wote wawili, lakini ikawa hajaingia peponi,’ na nikasema, ‘Aamiyn’. Baadaye akasema, ‘amekula khasara yule ambaye  wakati unapotajwa ikawa yupo na asikutakie Rehma juu yako,’ na nikasema, ‘Aamiyn’.”
Imepokelewa na Ibn Khuzaymah, 1888; at-Tirmidhiy, 3545; Ahmad, 7444; Ibn Hibbaan, 908. Angalia Sahiih al-Jaami’, 3501.

3 – Wafundishe (watoto) adabu nzuri na namna ya kula, kwa mfano kula kwa kutumia mkono wa kulia na kunywa kwa  kutumia mkono wa kulia na kuchukua chakula kutoka mbele ya nafasi zao (wasichukue upande wa mwengine); wakumbushe kwamba kufanya israfu  katika  chakula ni Haraamu na ni madhara kwa mwili.

4 – Usiwaachie kutumia wakati mrefu katika kula futari ikafikia hadi wakakosa Swalah ya jamaa ya Maghribi.

5 – Wakumbushe kuhusu hali za masikini na mafaqiri ambao hawawezi kumudu hata tonge ya chakula angalau wakaondosha moto wa njaa yao; Wakumbushe hali za wale wote ambao aidha huhama au hupigania Jihadi kwa ajili ya kutaka ridhaa ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) katika sehemu zote.

6 – Mikusanyiko hii (ya mwezi wa Ramadhwaan) inatoa nafasi nzuri ya kuwajumuisha jamaa pamoja na kuthibitisha mshikamano wa koo.  Mazoea kama haya yapo katika baadhi ya nchi, na vile vile ni nafasi nzuri ya kupatanisha na kutengeneza uhusiano uliovunjika baina ya jamaa.

7 – Inamsaidia mama (kupata nafasi nzuri ya) kutayarisha chakula,  kusafisha na vilevile kukiweka chakula muweko unaostahiki.

8 –Wawahimize watoto kuswali Swalah ya Taraawiyh na kujiandaa kwa ajili ya hiyo Swalah kwa kutokula sana na kujiweka tayari kwa wakati ili kwenda msikitini.

9 – Kwa kuzingatia Daku, wazazi ni lazima wawafundishe watoto baraka za daku na kwamba daku humpa mtu nguvu ya kufunga.

10 – Waruhusu kuwa na wakati wa kutosha kabla ya Swalah ya Alfajir ili kwa wale ambao hawakuswali Swalah ya Witri waweze kufanya hivyo kwenye wakati ule,  na vile vile kwa wale wanaochelewesha Swalah zao hadi wakati wa mwisho wa usiku, waweze kusali na pia kila mmoja aweze kuomba du’aa kwa Allaah vyovyote vile mtu apendavyo.

11 – Pawepo mazingatio ya kwenda msikitini kwa ajili ya Swalah ya jamaa ya Alfajir, kwa wale wanaowajibika kufanya hivyo. Tunaona watu wengine ambao huamka katika mwisho wa usiku kwa ajili ya kula daku, huwa wanarejea tena kulala na kupuuza (kupitwa) na Swalah ya Afajir.

12 – Ilikuwa ni kawaida ya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) katika kumi la mwisho la mwezi wa Ramadhani kukesha usiku na kuwaamsha watu wake. Hii inamaanisha kwamba familia ni lazima izingatie   kufanya jitihada kwenye wakati huu  adhimu (wenye baraka) ili kufanya matendo ambayo yanamridhisha Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala), huenda mtu Akatukuzwa na Kupandishwa daraja (za Amali zake njema). Kwa hivyo Mume ni lazima awaamshe Mkewe na Watoto wake ili kuyafanya yale ambayo yatawapelekea kuwa karibu na Mola Wetu (Subhaanahu wa Ta’ala).

13 – Hutokezeya wakati mwengine ikawa kuna watoto wadogo katika nyumba ambao wanahitaji kupewa moyo ili waweze kufunga, kwa hivyo baba ni lazima awahimize kuamka kwa ajili ya kula daku, na vile vile awape moyo kwa kuwasifu na kuwatunukia pindi wakimaliza mwezi mzima au hata wakifikisha nusu yake,  na vinginevyo (robo ya mwezi au wiki moja).
WALLAAHU AALAM

(MWENYEZIMUNGU NDIYE AJUWAE ZAID)