Mwezi mtukufu wa Ramadhani umegawanyika katika makundi matatu ambayo yana siku kumi kila moja, na kila kundi moja la kumi lina faida zak...
Mwezi mtukufu wa Ramadhani
umegawanyika katika makundi matatu ambayo yana siku kumi kila moja, na
kila kundi moja la kumi lina faida zake kwa mwenye kutimiza kile
kilichoagizwa na Mwenyezi Mungu.
Kumi la kwanza linajulikana kwa
jina la Rehma (rehema), la pili Magh-fira (kusamehewa madhambi) na lile
la mwisho linaitwa kumi la kuachwa huru na moto.
Katika kipindi hiki cha Mwezi
Mtukufu wa Ramadhani vitu vinavyopaswa kufanywa zaidi ni kuswali, kutoa
zaka na matendo mengine ambayo kwa kiasi kikubwa humpwekesha Mwenyezi
Mungu.
Katika mwezi huu, kila jema
analofanya mja hulipwa zaidi kuliko ambavyo analipwa katika siku za
kawaida, ndiyo maana watu hufurika kwa wingi katika nyumba za ibada.
Kumi la Rehma hupata baraka na kwa kila nachokifanya huku shetani akifungwa minyororo ili asiweze kuwarubuni watu.
Mtu mwenye kutimiza yale
yanayotakiwa katika kumi hili, hupata thawabu nyingi pamoja na
kujifungulia milango ya kuingia katika kumi la pili ambalo ni Magh-fira.
Wanazuoni na hadithi mbalimbali
zinatanabaisha kuwa, mtu mwenye kufanya ibada na kusoma kitabu kitukufu
cha Qur-an katika mwezi huu, husamehewa dhambi zake zote alizozitenda
huko nyuma.
Kumi la mwisho ni la kuachwa
huru na moto, ambapo waja ambao wametenda mema katika makumi
yaliyotangulia, huondolewa adhabu zote zilizokuwa zikimkabili siku ya
kiama.
Katika kumi hili la mwisho,
Waislamu hutakiwa kukesha zaidi katika nyumba za ibada kwa kuwa ndipo
hupatikana usiku mtukufu ambapo kitabu cha Qur-an kilishushwa (Laila-tul
Kadir)
Kwa mujibu wa vitabu mbalimbali
vya dini Malaika hushuka ardhini kutafuta watu wenye kusoma Qur-an au
kufanya ibada mbalimbali ambazo humpwekesha Mwenyezi Mungu.
Mja yeyote ambaye Malaika
wakimkuta akifanya ibada na kusoma Qur-an, huwa mwenye kupata daraja ya
juu kwa Mwenyezi Mungu pamoja na kufunguliwa mambo yake mengi ambayo
yalikuwa yamekwazika.
imsingi mwezi huu ni wa mchumo
kwa mja, kwa kuwa kila jambo jema analolifanya hulipwa maradufu
(thawabu) na kwa mwenye kufanya maasi hakika atakuwa ni mtu mwenye kula
hasara mbele ya Mungu na anakabiliwa na adhabu kubwa siku ya kiama.
Mwezi huu ni kama chuo cha
mafunzo ambapo baada ya kumalizika, waumini wanapaswa wawe wameelimika
na kubadilika ili wawe kama wamezaliwa upya kutokana na kutakasika na
maovu.
Haitarajiwi hata kidogo kwa
ambaye amejinyima kula (amefunga), kufanya ibada, kusoma Qur-an na mambo
mengine mema, kuanza kufanya maasi mara baada ya kumalizika kwa mwezi
huu.
Imekuwa desturi kwa baadhi ya
Waislamu kuuthamini na kuuona mwezi mtukufu wa Ramadhani ndiyo pekee wa
kumuabudu Mwenyezi Mungu na kufanya amali njema huku wakiiona miezi
mingine kama wamehalalishiwa kufanya maasi.
Dhana hii inapaswa kuachwa kwa
kuwa haitakuwa na maana kama muumini aliyepita katika chuo cha mafunzo
(Ramadhani) akalingana au kumzidi yule asiyepitia katika chuo hicho.
Mwenye kurejea kufanya maasi
mara baada ya Ramadhani, atakuwa ni sawa na mtu aliyejisafisha vizuri na
kuvaa nguo nyeupe, kisha akajirusha kwenye matope.
Kila kitu hujengwa na misingi,
mihimili au nguzo zinazokifanya kusimama imara. Mathalani, Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania inajengwa na mihimili mikuu mitatu, Utawala, Bunge
na Mahakama ambavyo aghalabu vyote hufanya kazi kwa kutegemeana.
Misingi ya Kiislamu, nayo
hujengwa na nguzo kuu tano ambazo kwanza ni kushuhudia kuwa na imani
kuwa hapana Mola anayepaswa kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu
mmoja na kwamba Mtume Muhammad (Rehema na amani zimfikie) ni mjumbe wa
Mwenyezi Mungu.
Nguzo ya pili ni kusimamisha
swala tano kwa maana ya kudumu kutekeleza ibada hiyo, yaani Adhuhuri
(saa 7 mchana), Alasiri (saa 10 alasiri), Magharibi (saa 12 jioni),
Insha (saa 2 usiku) na Alfajiri (saa 11 alfajiri) na ya tatu ni kutoa
zaka kwa wenye uwezo.
Mihimili mingine miwili ya
Uislamu baada ya Shahada, Swala na Zaka ni kufunga Mwezi Mtukufu wa
Ramadhani, nguzo ambayo ndiyo kiini cha makala hii, na ya mwisho ni
Hijja, ambapo waumini wenye kuweza wanakwenda kuhiji katika nyumba ya
Mwenyezi Mungu huko Makkah, Saudi Arabia.
Nawatakia wote funga njema ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
MUNGU NDIYE AJUAYE ZAIDI
ASANTE.
COMMENTS