VIPI UNAWEZA KUISOMA QUR’AN YOTE NDANI YA MWEZI WA RAMADHANI? Assalam alaykum warahmatullah wabaraqatuh. S...
VIPI UNAWEZA KUISOMA QUR’AN YOTE NDANI YA MWEZI WA RAMADHANI?
Assalam alaykum warahmatullah wabaraqatuh. Sifa zote njema Anastahiki Allah(S.W) Muumba wa mbingu na ardhi na vyote vilivyomo ndani yake. Yeye tu ndiye anastahiki kuabudiwa, kuombwa na kunyenyekewa. Hapana mola isipokuwa yeye. Rehma na amani zimfikie mtume Muhammad (S.A.W) ahli zake,maswahaba wake na wote wanaomfuata kwa wema hadi siku ya mwisho.
Habari za swaum? Ni matumaini yangu kwamba mu wazima wa afya kwa uwezo wake Allah (S.W). Kwa wale ambao hawajisikii vyema Allah (S.W) Awape afua waweze kuufunga mwezi huu mtukufu wa Ramadhani.
Ndugu zangu waislam,tupo katika mwezi mtukufu wa Ramadhani,mwezi wa neema na baraka tele. Mwezi ulioshushwa Qur’an ndani yake, ili iwe muongozo kwa watu. (Qur’an; 2:185)Ni jambo lenye kupendeza, na ni sunnah ilokokotezwa kusoma Qur’an ndani ya mwezi huu, hususan nyakati za usiku.
Katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhani, malaika Jibril alikuwa akishuka na kuja kumfunza mtume Muhammad (S.A.W) kusoma Qur’an(Sahih Bukhari mlango wa kwanza,kitabu cha kwanza, Hadith 5). Hii inaonesha umuhimu wa kusoma Qur’an tukufu,hususan mwezi huu mtukufu wa Ramadhan, ambapo Allah (S.W) kwa makusudi kabisa alikuwa akimtuma malaika wake Jibril kuja kwa kipenzi chake mtume Muhammad (S.A.W) kila usiku wa Ramadhan kuja kumfunza kuisoma Qur’an.
Kusoma Qur’an katika mwezi wa Ramadhan kuna fadhila kubwa sana,kwanza ni kuadhimisha kushushwa kwake,pili ni kuifata sunnah ya mtume (S.A.W) na rafiki yake malaika Jibril walivyokuwa wakifanya kila usiku wa Ramadhani. Na la tatu ambalo ni kubwa zaidi Mtume (S.A.W) Anasema ‘someni Qur’an kwani itakuwa shifaa’a (muombezi) siku ya Qiyama. Na katika hadithi nyingine Anasema bwana Mtume (S.A.W) “Swaum na Qur’an vitamuombea mtu siku ya Qiyama. Swaum itasema,Mola wangu nilimzuia kula na kunywa, sasa leo niache nimuombee shifaa’a. Na Qur’an nayo itasema nilimzuia kulala, Mola wangu, sasa leo niache nimuombee shifaa’a. Na Allah (S.W) Atairuhusu funga na Qur’an iweze kuwa muombezi kwa mja huyo” (Sahih Muslim)
Hivyo basi ndugu yangu muislam ni vyema tukajihimiza kusoma Qur’an ndani ya mwezi huu mtukufu wa Ramadhan. Sasa tuangalie je ni vipi tunaweza kuisoma Qur’an yote ndani ya mwezi huu wa Ramadhani.
Qur’an ina juzuu thelathini sawa na siku thelathini za mwezi, hivyo kwa kusoma juzuu moja kila siku inatosha kutimiza Qur’an yote kwa mwezi. Tukumbuke pia Qur’an (mas’haf) ina kurasa kati ya 604– 612. Inahitaji kusoma kurasa ishirini kwa siku kwa muda wa siku thelathini kumaliza msahafu mzima. Siku moja ina swala tano, tukizigawa kurasa ishirini kwa swala tano tunapata kurasa nne katika kila swala. Tukigawa kurasa nne kwa mbili, yaani itakuwa kurasa mbili kabla ya swala na mbili baada ya swala, ni kiasi chepesi kwa mtu kuisoma Qur’an nzima ndani ya mwezi.
Kwa wale ambao hawana muda wa kusoma kurasa nne kila swala, hebu tujaribu hii. Tusome kurasa saba baada ya swala ya sub’hi (alfajir), saba baada ya swala ya laasiri na saba baada ya taraweeh (swala ya Isha). Hivyo itakuwa saba mara tatu ambayo ni sawa na 21. 21 mara siku thelathini ni 630 yaani msahafu na zaidi.
Tukumbuke tabia hujenga mazoea, hebu tuchague hesabu moja na tuanze nayo mazoezi katika maisha yetu. Mwisho wa siku tutazoea na litakuwa jambo jepesi kwetu na la kawaida. Tukumbuke mtume (S.A.W) Anasema kila herufi moja ya Qur’an ina thawabu kumi, Qur’an nzima ina herufi 323,670 ,hivyo basi kila mwezi utakuwa umejiwekea akiba ya thawabu 3,236,700, yaani 323,670 x 10=3,236,700.
Mungu ndiye ajuwae zaidi
IMENAKILIWA NA sayyidbunduki.blogspot.com
kutoka katika vyanzo vyenye kuaminika.
COMMENTS