Maneno ya mkosaji, hayachagui sehemu
Nchi kavu kwenye maji, popote hutia timu
Leo nami msemaji, nawausia kaumu
Kamata wosia wangu, ukiona unamana
Ndugu zangu wasomaji, sikia hii ilimu
Siku zote mfamaji, kutapatapa muhimu
Leo nami msemaji, nawausia kaumu
Kamata wosia wangu, ukiona unamana
ishi na watu vizuri, Mungu atakubariki
ukijiona mzuri, mwenzako simdhihaki
kama kwako mambo shwari, muhishimu mwenye dhiki
Kamata wosia wangu, ukiona unamana
Msichana mwenye ndoa, simdharau mjane
Usije mtia doa,usiombe mufanane
Kwake ukajitanua, kwa marefu na manene
Kamata wosia wangu, ukiona unamana
Usimcheke kilema, kwa kukosa utimamu
Ni kazi yake Karima, ndiye mshika hatamu
Sidharau mkulima, ukiwa DARI SALAMU
Kamata wosia wangu, ukiona unamana
Wanaume waungwana, ka elimu chukueni
Usitake msichana, kumbe hayupo kichwani
Aweza kupenda sana, kamtia adhabuni
Kamata wosia wangu, ukiona unamana
Usijaribu mapenzi, mpana wake uwanja
Mapenzi ni kikohozi, kijaribu utabanja
Changanua hii kozi, ukifosi utahanja
Kamata wosia wangu, ukiona unamana
Jua ndoa kisha oa, ndoa si kwenda chooni
Tafakari kisha oa, jibu toka akilini
Sikurupuke kuoa, wallahi mwisho tanzini
Kamata wosia wangu, ukiona unamana
Usimdharau mtu, yeyote umuonae
Siri ya mtu msitu, Mola ndiye ajuwae
Usikadirie katu, hwenda hupo sawa nae
Kamata wosia wangu, ukiona unamana
Zichunge zako lahaja, walimwengu wana mambo
Watu wana madaraja, na wengine wapo ng’ambo
Chunga kauli yo mja, mwanajeshi na mgambo
Kamata wosia wangu, ukiona unamana
Kazi ya mtu heshimu, cha haramu mkosoe
Akihitaji elimu, mfahamishe ajue
Usijikute hakimu, kujiona wewe ndie
Kamata wosia wangu, ukiona unamana
asante sana
COMMENTS