"KUSAMEHEANA NA FAIDA ZAKE" Kila sifa njema zinamstahikia Allah Mola wa viumbe vyote. Sala na salamu zimuendee Mtume wetu Muha...
"KUSAMEHEANA NA FAIDA ZAKE"
Kila sifa njema zinamstahikia Allah Mola wa viumbe vyote. Sala na salamu
zimuendee Mtume wetu Muhammad (swalla Allahu alaihi wa sallam) na ahli
zake na maswahaba wake.
Kwa hakika mwanadamu ni kiumbe dhaifu sana. Na udhaifu wake
huanza kuonesha kwa mola wake kwa kumuasi. Hakuna kiumbe yeyote yule
anaeweza kuishi katika ulimwengu huu bila ya kumuasi Allah (subhanahu
wataala). Ila Allah (subhanahu wataala) akatuwekea milango ya tawba wazi
ili wale wenye kumkosea Allah waweze kurudi kwake na waombe msamaha.
Vile vile udhaifu wa binaadamu anauonesha tena baina yake na binaadamu
wenzake. Hakuna mwanaadamu anaeweza kukaa na mwanadamu mwenzake bila ya
kumkosea. Sote tunakoseana. Ila suala linakuja je baada ya kukosana
tuache tu ? Hapana. Lazima baada ya kukosana tuombane msamaha na
tusameheane ili tuyaondoshe yale yaliyomo ndani ya nyoyo zetu. Kufanya
hivyo kutatufanya sisi tuweze kuishi kwa uzuri. Jambo la kusameheana
baina ya watu limezungumziwa na Allah (subhanahu wataala) pale aliposema
ndani ya Quraan “na wanajizuia ghadhabu, na wasamehevu kwa watu; na
Mwenyezi Mungu huwapenda wafanyao wema”(3:134). Kuzuia ghadhabu zako na
kumsamehe yule aliyekukosea ni katika wema na mwenye kufanya wema basi
hupendwa na Allah (subhanahu wataala). Je kweli hatutaki kupendwa na
Allah ? Na usipopendwa na Allah vipi utaishi katika ulimwengu huu? Vipi
utaikabili akhera yako? Pia katika aya nyengine Allah (subhanahu
wataala)anasema “Shikamana na kusamehe, na amrisha mema, na jitenge na
majahili (wajinga)” (Al-Araaf 7: 199)
.
Ugomvi uko kila sehemu na takriban kwa watu wengi sana ila
tukimbilie kusameheana ili turejeshe mapenzi baina yetu. Kusamehe kuko
kwa namna tatu kuu, namna ya kwanza ni kumsamehe ndugu yako yule
aliyekuomba msamaha kutokana na lile alilolifanya. Pili ni kumsamehe
ndugu yako hata kama hajakuomba msamaha. Na tatu ambako kuliko kuwa bora
zaidi ni kumuomba wewe msamaha ndugu yako aliyekukosea wewe baada ya
kuona hajui kosa lake au kwa kujua na akashindwa kukuomba msamaha.
Ndugu yangu muislamu unapomkosea ndugu yako basi kimbilia
kumuomba radhi kutokana na lile ulolifanya. Kumuomba radhi muislamu
mwenzako hakukushushi cheo wala hadhi. Bali hukupandisha darja zaidi na
kuonesha utu na uungwana uliokuwa nao kutokana na kuufahamu vizuri
uislamu wako. Pia anapokuja ndugu yako kukuomba msamaha usimrudishe bila
ya kumsamehe kwa sababu sisi tunamuasi mangapi Allah tunajua kama haya
ni makosa na tunamuasi ila tukirudi kwake anatusamehe. Hivyo basi na
sisi tusimpe sheytwan nafasi katika kutufarakanisha. Na wala usiwe
mwenye kujinadi kwa watu kuwa wewe ni bora na ndio maana unaombwa radhi.
Yote hayo tuyafanye kwa ajili Allah (subhanahu wataala). Ukiyafanya kwa
ajili ya Allah hutokuwa na kiburi,wala majivuno ndani na nje ya nafsi
yako.
Je ni zipi faida za waislamu kusameheana baina yetu?
1-Kupendwa na Allah (subhanahu wataala)
Allah (subhanahu wataala) anasema ndani ya Quraan “na
wanajizuia ghadhabu, na wasamehevu kwa watu; na Mwenyezi Mungu huwapenda
wafanyao wema”(3:134). Kuzuia ghadhabu zako na kumsamehe yule
aliyekukosea ni katika wema na mwenye kufanya wema basi hupendwa na
Allah (subhanahu wataala). Na bila ya shaka muumini ndani ya ulimwengu
huu huhitaji mapenzi na radhi za Allah. Hivyo katika njia ya kuzipata
radhi za Allah ni kusameheana baina yetu.
2- Kujenga mapenzi ,umoja baina ya familia na kuunga udugu.
Katika matatizo makubwa yanayokumbuka familia zetu sasa
hivi ni kukithiri kwa ugomvi ndani ya familia. Na bahati mbaya zaidi
watu wengi hawatafuti njia za kusuluhisha bali huzidisha zaidi na
kuchochea ugomvi ule. Ugomvi husababishwa aidha kwa mali,wake, watoto
n.k. Ndugu zangu wa kiislamu panapotokea ugomvi baina ya familia basi
pasuluhishwe ugomvi huo. Ili ugomvi huo uondoshwe. Kuweko kwa ugomvi
ndani ya familia kutapelekea kukosa mapenzi baina yao, kukosa
kuhurumiana baina yao na mwisho kutapelekea kukatika kwa familia ile. Na
je tunajua ni ipi adhabu ya mwenye kukata ukoo ? Mtume (swalla Allahu
alayhi wasallam) anasema “Haingii peponi mwenye kukata udugu” Bukhary
na Muslim. Kwa hakika tunaitaka pepo ya Allah hivyo basi tuwe wepesi
kuombana msamahan na tusameheane. Na ikiwa moja kati yenu hajaomba
msamaha kwa kukhofia kutoipata pepo ya Allah basi muumini wa kweli
anatakiwa akamfuate ndugu yake waombane msamahana wasameheane ili waweze
kuondosha tofauti baina yao.
3- Kujenga na kurejesha mapenzi baina ya wanandoa.
Ndoa nazo zina dhoruba ya ugomvi wa kila mara.
Panapotokezea ugomvi baina ya wanandoa kitu muhimu zaidi ni subra.
Baada ya kuwepo subra basi waombane radhi baina ya mke na mume. Kwa
hakika mke au mume anapoombwa radhi na mwenzake huwa na furaha na
hulainika moyo wake. Kulainika kwa moyo wake kunapelekea kutuliza ugomvi
ule na kurejesha tena mapenzi baina yao. Nasaha zangu kwa wanandoa
kusiwe na hata mmoja kati yao ambae atakuwa anaona tabu kumuomba
samahani mwenzake. Na wala mume asijione kuwa yeye tu ndie anaestahiki
kuombwa radhi.
Mume akikosea amuombe radhi mkewe na mke akikosea amuombe
radhi mume. Je unajua utamu wa neno samahani kwa mke au mume pale
wanapokosana. Hebu jaribu kutumia fursa ya kuombana radhi kila
punapokosana ili muifanye ndoa yenu iwe imara. Na inapendeza zaidi mmoja
wao akimuomba mwenzake samahani huku akimpa zawadi kwa uwezo alojaaliwa
bila ya kujikalifisha, au mke kumpikia mume chakula kizuri. Na wewe
unaeombwa samahani usirejeshe samahani kurudi tupu msamehe kwani
kusameheana ni wema katika uislamu na unapata thawabu kwa wema huo.
4- Kujenga mapenzi baina ya majirani na kupelekea kuishi kwa amani katika nyumba zetu.
Majirani wale waliokosana wasameheane kwa yale
yaliyotokezea. Na msamehe jirani ikiwa amekuomba radhi au hajakuomba
radhi. Jirani ana haki kubwa sana ndani ya uislamu na muislamu ajue pale
jirani yake anapokosa kusalimika kutokana na maneno yake au vitimbi
vyake basi hatoingia peponi kwa ushahidi wa hadithi ya Mtume (swalla
Allahu alayhi wasallam) Mtume (swalla Allaahu alayhi wasallam)
aliulizwa,“Mwanamke fulani namkumbuka kwa wingi wa Swalah zake, Saumu
zake na sadaka zake azitoazo lakini anawaudhi jirani zake kwa ulimi
wake.Mtume (swalla Allaahu alayhi wasallam) akajibu, ‘Kwa hakika yeye ni
mtu wa motoni”. Imepokea na Imam Ahmad . Hivyo ndugu yangu wa kiislamu
msamehe jirani yako kwa kosa alilokufanyia kwa kujua au kutokujua, kwa
kukuomba radhi au kutokuomba radhi.
5- Kusameheana baina ya waislamu wawili kunapelekea kujiepusha na makatazo ya Allah.
Kusameheana vipi kutatufanya tujiepushe na makatazo ya
Allah ? Mtume (swalla Allahu alayhi wasallam) anasema “ Si halali kwa
muislamu amhame ndugu yake wa kiislamu zaidi ya siku tatu, hata
wanapokutana huyu anamgeuzia (uso) huyu na huyu anamgeuzia (uso) huyu.
Na aliye mbora wao ni yule anayeanza kutoa salaam”.Bukhari na Muslim.
Na katika riwaya nyengine "Atakayemhama (mwenzake) zaidi ya siku tatu
akafariki, basi ataingia motoni" Abuu Daud. Hivyo basi ndugu zangu wa
kiislamu kwanza tuwe wenye kuombana radhi pale tunapokosana na pia tuwe
wenye kusameheana na ikiwa ndugu yako amekukosea na kama hajakuomba
radhi basi msamehe ili uwe mbali na kumuasi Allah (subhanahu wataala).
6- Kupata kivuli cha Allah (subhanahu wataala)
Haya yameelezwa na Mtume (swalla Allahu alayhi wasallam)
pale alipowafundisha waislamu awe mwenye kumvumulia ndugu yake muislamu
kutokana na deni au amsamehe basi atapata kivuli siku ambayo hakutokuwa
na kivuli ila cha Allah. Imepokelewa kutoka kwa Abu Hurayrah(radhi za
Allah ziwe juu yake) amesema: “Mtume wa Allaah (swalla Allahu alayhi
wasallam) amesema: "Atakayemuakhirishia mwenye usiri (wa kulipa deni) au
akamsamehe, Allah Atamfunika kivuli Siku ya Qiyaamah chini ya kivuli
cha Arshi yake, siku ambayo hakutakuwa na kivuli isipokuwa kivuli Chake.
Attirmidhy. Na Allah (subhanahu wataala) anasema “Na ikiwa (mdaiwa) ni
mwenye hali ngumu, basi (mdai) angoje muda wa kufarijika (anayemdai).
Na mkitoa swadaqah (deni mnalodai) basi ni kheri kwenu mkiwa mnajua”
(2:280).
Mwisho kabisa nimalizie mada yangu kwa kisa kinachotufunza kuhusu kusameheana.
Mwisho kabisa nimalizie mada yangu kwa kisa kinachotufunza kuhusu kusameheana.
Vijana watatu walikwenda mbele ya Khalifa wa Waislamu
Umar bin Al Khattab (Radhiya Llahu anhu) wakiwa wamemkamata mtu
waliyemfunga kamba. Wakasema kumwambia Umar (Radhiya Llahu anhu):
"Mtu huyu amemuuwa baba yetu na amekiri juu ya jambo hilo,
isipokuwa ametuomba tumpe siku tatu ili aweze kusafiri kwa wanawe kwa
ajili ya kuwajulisha juu ya hazina aliyoifukia mahala ambapo hapana
anayepajuwa isipokuwa yeye peke yake". Sahaba mmoja aitwae Abu Dhar Al
Ghafariy (Radhiya Llahu anhu) akamdhamini mtu huyo juu ya kuelewa kwake
vizuri kuwa iwapo mtu huyo hatorudi basi atauliwa yeye badala yake. Mtu
huyo hakurudi mpaka baada ya kukaribia sana kumalizika muda wa siku tatu
hizo, na watu wakawa na wasi wasi asije Abu Dhar (Radhiya Llahu anhu)
akauliwa badala yake.
Dakika za mwisho za siku ya tatu akawasili mtu huyo akiwa
amejaa vumbi na huku uso wake ukionesha dalili za kuchoka sana. Umar
(Radhiya Llahu anhu)akamuuliza: "Ilikuwaje ukarudi wakati ungeweza
kukimbia?" Akajibu: "Nilihofia pasije pakasemwa kuwa; Watu wenye ahadi
za kweli hawapo tena."
Kisha Umar (Radhiya Llahu anhu)akamgeukia Abu Dhar
(Radhiya Llahu anhu)na kumuuliza: "Na wewe ilikuwaje ukakubali
kumdhamini mtu huyu wakati humjuwi?" Abu Dhar (Radhiya Llahu
anhu)akasema: "Nilihofia pasije pakasemwa; Wakarimu na wenye moyo wa
kishujaa hawapo tena."
Ndipo wale vijana watatu wakasema: "Na sisi tumemsamehe
mtu huyu ili pasije pakasemwa; 'Hawapo tena watu wenye kusamehe juu ya
kuwa na uwezo wa kulipa kisasi."
Familia,majirani,marafiki au baina ya waislamu ombaneni
msamaha na kila mmoja amsamehe mwenzake kwa yaliyopita. Na yafanyeni
hayo kwa ajili ya Allah (subhanahu wataala).
Allah atujaalie tuwe kuyafahamu haya yote tuliyoyaeleza. Na
tuchukue manufaa yake kwa kusameheana baina yetu ili tuweze kuishi kwa
mapenzi na salama baina yetu. Aaamin

COMMENTS