Unajifanya waringa, waringa nini ARAFA Umbo la kuunga unga, lakini huishi sifa Leo fundi nakuganga, husiano litakufa Kitu gani waring...
Unajifanya waringa, waringa nini ARAFA
Umbo la kuunga unga, lakini huishi sifa
Leo fundi nakuganga, husiano litakufa
Kitu gani waringia, mpaka kuninyanyasa?
Umbo lako la mkunga, mrefu kama gorofa
Miguu kama kinyonga, mwili umejaa nyufa
Vijikono kama panga, una kata si tarafa
Kitu gani waringia, mpaka kuninyanyasa?
Huna rangi huna sura, si mtu sio kinyago
Huna nyonga huna chura, miguu kama mtego
Kibichwa kama mpira, hakibandiki mziogo
Kitu gani waringia, mpaka kuninyanyasa?
Ukenda kama warudi, ukisimama wayumba
Sauti kama ya radi, ngozi yako kama mamba
Ulojawa na hasadi, wakusumbua ushamba
Kitu gani waringia, mpaka kuninyanyasa?
Si kila akutakae, atakuwa akupenda
Ukae ufikirie, utajifunza huenda
Watoto akulelee, na kutaka kukulinda
Kitu gani waringia, mpaka kuninyanyasa?
Nilikuomba nakiri, mapenzi nilikutaka
Lakini kwanza fikiri, wewe ulishaachika
Lengo ni kukusitiri, watoto wangeteseka
Kitu gani waringia, mpaka kuninyanyasa?
Mapenzi kitu khiyari, hilo linafahamika
Ngekuwa huko tayari, ungenambia hakika
Sikukutia kabari, mwenyewe lilainikia
Kitu gani waringia, mpaka kuninyanyasa?
Mimi ni mtu mzima, sio wa kidigitali
Nilikwonea huruma, ingawaje sina mali
Kidogo nitachochuma, chatosha japo ugali
Kitu gani waringia, mpaka kuninyanyasa?
Imeniponza hekima, imegeuka muhali
Bora ningekwacha wima, ukapambana na hali
Lakini zangu huruma, leo wanilaza chali?
Kitu gani waringia, mpaka kuninyanyasa?
Alokwacha ni timamu, alichoka tabiazo
Wala usimlaumu, wewe ndiye hamnazo
Mimi sitokuhukumu, kwangu ondoa mawazo
Kitu gani waringia, mpaka kuninyanyasa?
Nakuonya sikiliza, kisha yafanyie kazi
Yako sitozungumza, mimi sio domo wazi
Kaza buti kisha kaza, mimi naachia ngazi
Kitu gani waringia, mpaka kuninyanyasa?
Najua umetosheka, unaniona wa kale
Utakuja nikumbuka, masiku ya huko mbele
Napoteza zangu chaka, kuvua zangu kambale
Mungu atakuonesha,
dunia si mama yako.
COMMENTS