Assalamu alaykum warahmatullahi wabarakatuh. Karibuni wasikilizaji wapenzi katika kipindi hiki maalumu nilichokuandalieni kwa mnasaba w...
Assalamu alaykum warahmatullahi wabarakatuh. Karibuni wasikilizaji wapenzi katika kipindi hiki maalumu nilichokuandalieni kwa mnasaba wa mwezi mtukufu wa Ramadhani ambacho kwa leo kitaanza kwa kugusia falsafa na hekima ya funga.
Kuhusu
falsafa na hekima ya funga au saumu yamezungumzwa mengi ndani ya
Qur’ani tukufu, Hadithi pamoja na kauli za maulamaa wa dini. Katika
kubainisha hukumu ya kufaradhishwa na kuwajibishwa kufunga, Qur’ani
tukufu imeitaja taqwa na uchaMungu kuwa moja ya hekima za kufaradhishwa
amali hiyo tukufu. Aya ya 183 ya Suratul Baqarah inasema:
Enyi mlio amini! Mmeandikiwa Saumu, kama walivyo andikiwa walio kuwa kabla yenu ili mpate kuchamngu.
Funga
ni moja ya amali bora kabisa za kumwezesha muumini kudhibiti ghariza za
kihayawani na kuhuisha moyo wa uchaji Mungu ndani ya nafsi yake. Kama
ilivyoelezwa katika Hadithi ni kwamba: “Funga ni ngao (ya Moto wa
Jahannamu)”. Yaani mtu atanusurika na kuokoka na Moto wa Jahannamu
kutokana na kufunga. Na sababu ni kuwa, kutokana na t’aa, ibada
anazofanya mtu na kuzidhibiti na kuzidhoofisha hawaa na matamanio ya
nafsi hatimaye huweza kumdhibiti na kumshinda shetani wa ndani na nje ya
nafsi yake. Na ni kutokana na hayo ndipo Bwana Mtume Muhammad SAW
akasema: “Ndani ya mwezi huu mashetani hufungwa pingu na minyororo, basi
mwombeni Mwenyezi Mungu asiwasalitishe juu yenu”.
Kwa
mujibu wa aya za Qur’ani tukufu, shetani ameapa kuwa atawapotosha na
kuwatoa nje ya mkondo wa njia iliyonyooka waja wote wa Mwenyezi Mungu
isipokuwa wale ambao ni “mukhlasin”. Kwa hivyo kila mja ambaye
anamwomba na kumwabudu Allah kwa ikhlasi, shetani hatokuwa na nguvu juu
yake. Na sababu ni kuwa, kama ambavyo maji na moto havitangamani,
kumdhukuru na kumtaja Allah kunakinzana na wasiwasi wa shetani; na vitu
viwili vyenye mgongano haviwezi kujumuika pamoja. Kwa hivyo maana ya
kufungwa mikono na miguu mashetani kwa minyororo ni kwamba katika mwezi
mtukufu wa Ramadhani, dhikri, dua na utajo wa Allah huwa mkubwa na
mwingi kiasi ambacho haibakii tena fursa yoyote ile kwa wasiwasi wa
shetani aliyebaidishwa na rehma za Allah.
Wapenzi
wasikilizaji, maana ya funga au saumu kilugha ni kujizuia na kila kitu;
na katika istilahi za fiqhi maana yake ni kujizuia na mambo manane
ikiwemo kula na kunywa kuanzia alfajiri hadi magharibi kwa nia na
kusudio la kutekeleza amri ya Mwenyezi Mungu. Mtu ambaye amechunga
hukumu za dhahiri na za kifiqhi za funga, funga yake huwa imesihi
kisheria. Lakini ili funga na saumu yake ikubalike na kupata malipo ya
thawabu mbele ya Mwenyezi Mungu kuna masharti yanayomlazimu kutekeleza.
Funga inayotakabaliwa ni ile inayomjenga na kumkuza mtu kimaanawi. Saumu
ya aina hiyo, mbali na kuchunga hukumu za funga, yaani kujizuia na kula
na kunywa na mengineyo, huandamana pia na kuviepusha viungo na mambo ya
haramu bali pia hata ya makruhu. Ikiwa mfungaji atapata taufiqi ya aina
hiyo, funga yake huwa imesihi na amali zake huwa zimetakabaliwa na
humuongoza kuelekea kwenye ukamilifu na kumkurubisha na Mwenyezi Mungu.
Maneno
haya ya Bwana Mtume yanabainisha kuwa kiwango na wingi wa ufanyaji
ibada wa mtu, hauwezi kuwa kipimo cha kuonyesha thamani na utukufu wake
na matunda ya juhudi zake; bali ubora na namna ya ufanyaji ibada wa mtu
ndio unaoakisi thamani na utukufu wake wa kimaanawi.
Imepokewa
Hadithi kwamba wanawake wawili walikuwa wamefunga saumu katika zama za
Bwana Mtume Muhammad SAW, lakini ulipokaribia wakati wa kufuturu hali
zao zilikuwa taabani kwa kiu na njaa kali. Kwa hali hiyo wakamtuma mtu
kwa Bwana Mtume SAW akawaombee ruhusa ya kufungua. Bwana Mtume Muhammad
SAW aliwapelekea chombo wanawake hao na kumwambia aliyewatuma: “Waambie
wavitapike vile walivyovila!” Kilichotokea ni kwamba nusu ya chombo kile
ilijaa mapande ya damu na nyama. Watu walipatwa na mshangao walipoona
hali ile. Bwana Mtume akawaambia: Wanawake hawa walijizuia na yale
ambayo yalikuwa halali kwao, na wakabatilisha funga zao kwa yale
waliyokuwa wameharamishiwa, kwa namna ambayo walikuwa wakikaa
kuwasengenya watu; kwa hivyo hivi vilivyomo ndani ya chombo hiki ndiyo
yale waliyokuwa wakiwasema watu!”
Wapenzi
wasikilizaji, tujitahidini sana kuzichunga ndimi zetu, macho na masikio
yetu na mambo yaliyoharamishwa ili tusije tukawa katika wale ambao
hawapati chochote katika funga zao zaidi ya kushinda na njaa na kiu.
Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.
COMMENTS