Kila nafsi itaonja mauti. Nami zamu yangu imefika hivyo naomba kuwaaga ndugu, jamaa na marafiki
Waungwana mi nakwenda, nishazipata habari
Maisha nimesha sanda, zimeshakwisha dahari
Ingawaje sikupenda, kuelekea kaburi
NAKWENDA
Nimeitwa na muumba, nakwenda siwezi pinga
Uhai umeshayumba, Maliki ameshapanga
Hizi beti nazoimba, leo ndo mwisho kutunga
NAKWENDA
Jina mtanibadili, punde muda si mrefu
Kifo kikinikabili, japo sio maarufu
Najua mtajadili, mazuri na madhaifu
NAKWENDA
Najua mtashituka, kusema najichuria
Lakini hiyo hakika, hiki nino waambia
Kwaherini dada kaka, msisite niombea
NAKWENDA
Nitawamis wa huku, hamtoweza nipata
Rafiki wa face book, wasap na kule twita
Maisha ni kama luku, duniani tunapita
NAKWENDA
Nilisema niuchune, nikashindwa vumilia
Nakwenda nikaonane, na waliotangulia
Nitamuacha mjane, mke wangu maridhia
NAKWENDA
Nakwenda imi nakwenda, na mimi sio wa kwanza
Hii ni kama ajenda, hivyo punguza kuwaza
E ndugu unonipenda, utapata maliwaza
NAKWENDA
Walikwenda tangu zama, ndugu jamaa wadau
Kama taa walizima, wakituacha na kiu
Ki ukweli inauma, nami mtanisahau?
NAKWENDA
Hata msonifahamu, ujumbe huu ufike
Nimepata ilhamu, ujumbe huu niweke-
Msije kunishutumu, Muumba ni kazi yake
NAKWENDA
Kumi beti ya tamati, bunduki huyo nasepa
Nakunja langu busati, navaa yangu malapa
Asante wanakamati, kwa umoja mlonipa
ILA HII NI SANAA