Hii ni historia ya kijana mmoja ambaye hakupenda jina lake liwekwe wazi. Anaeleza jinsi alivyoingia katika kumi na nane za wanajeshi huko Koko beach jijini DAR ES SALAAM.
Anasimulia Kama ifuatavyo;-
"Niliamua kumtembelea shangazi yangu ambaye alikuwa anaishi Dar es salaam. Sasa shangazi alikuwa anaishi maeneo fulani karibu na baharini.
Kwakuwa nilikuwa sijawahi kufika baharini siku moja niliamua kutembea na kwenda kujionea mawimbi murua ya bahari ya hindi. Ikumbukwe kwamba nilizaliwa na kukulia Mkoani SUMBAWANGA hivyo sikuwahi kuiona bahari live.
Siku moja baada ya shangazi kwenda kazini niliamua kutoroka na kwenda kutembea tembea maeneo ya pwani kupoteza mawazo kidogo. Nilikuwa muoga wa maji hivyo sikuwa na ujasiri wa kuyasogelea kwa ukaribu zaidi nikiogopa mawimbi yake.
Niliamua kutembea na ufukwe ule huku nikicheza kwa kukimbizana na wale wadudu wa baharini wanaoitwa KAA.
Nilifika maeneo ambayo yalikuwa na minazi miingi, kwa mbali upande wa baharini eneo ambalo lilikuwa limezungukwa na maji, niliona watu wakichukua mazoezi mbali mbali. Kwakuwa walikuwa mbali niliendelea na safari yangu bila kutaka kujua kuwa walikuwa ni watu gani.
Niliendelea na safari yangu kwenda kusiko julikana mpaka nilipokuja kushituka nilikutana na shuka na baadhi ya nguo za kijeshi zikiwa zimeanikwa baada ya kufuliwa.
Moyo ulipiga paaa....... Nikasema du kumbe hili Ni eneo la jeshi.?? Niliamua kugeuza na kurudi nilikotoka.
Baada ya kupiga hatua Kama kumi tu nilikutana uso kwa uso na mwanajeshi ambaye alikuwa amevaa sare na alikuwa amebeba bunduki. Kitu ambacho nakumbuka ni kwamba katika sare yake yalionekana maneno yaliyoandikwa kwa herufi nyekundu MP.
Yule mwanajeshi aliniita na akaniambia kuwa nimefikaje pale? Nilijitetea kuwa Mimi ni mgeni na sikujua kuwa pale ni kambi ya jeshi. Alitaka kujua kuwa nimetokea wapi? Lakini kabla sijamjibu nilikula makofi mawili ya nguvu sana ambayo yalinifanya nianze kuona nyota nyota na kujibu nikiwa na mawenge
Alitoa simu yake na kuwapigia wenzake ambao bila shaka walikuwa ni wale waliyokuwa wakichukua mazoezi kule nyuma nilikopita. Kumbe bwana wale walikuwa ni wanajeshi.
Laiti ningejua nisingekanyaga eneo lile mimi jamani. Niliijutia nafsi yangu kwa kujitorosha nyumbani na kuja pwani. Laiti ningejua ningekaa tu home.
Walipokuja wale wanajeshi wengine walikabidhiwa mimi rasmi kwa ajili ya kunitia adabu. Aisee nilipewa adhabu ya kuyachota maji ya bahari mpaka yaishe. Nilikuwa nayatoa kwenye dimbwi namba moja na kujaza dimbwi namba mbili.
Niliona ni adhabundogo lakini baadaye iliniwia uzito sana. Nilichota yale maji kama mda wa masaa mawili hivi, wakati huo wakiendelea kuniuliza maswali mbali mbali wakidhani moja kwa moja kuwa mimi ni mhamiaji haramu au gaidi. Hasa ukizingatia Mimi ni mweusi kupita kiasi. Aloo adhabu za kijeshi uzisikie hivyo hivyo rafiki yangu.
Baadaye walinibadilishia adhabu na kunivisha matairi ya gari na kuanza kuchuchumaa na kusimama nayo. Hapo nikitoa mchozi mtu mzima na kuomba msamaha lakini hawakunisikiliza. Baadaye tena walianza kunigaragaza kwenye maji na mchanga kwa muda mredu kweli. Daah kwakweli ile siku sitoisahau maishani mwangu.
Mwisho wa siku waliamua kuniachia lakini kwa shariti moja. Watanikimbizaaaa wakinikamata watanirudisha tena kwenye adhabu.
Baada ya kuachiwa katika adhabu ile iliyodumu kwa masaa takriban sita, niliachiwa, nikakimbilia sehemu ya juu ya pwani ya bahari ile palipo karibu na namakazi ya raia na kujilaza chini.
Kwakuwa nilikuwa nimejichokea sana nilipitiwa na usingizi mzitio kabla ya kushituliwa na kibaka aliyekuwa akinipapasa mifukoni.
Niliamka na yule kibaka alikurupuka na kusema kumbe hujakufa shenzi we. Jamaa akakimbia nami nikaamka na kurudi nyumbani Nikiwa hoi. Mpaka muda ule ilikuwa ni saa kumi na moja ya jioni tangu saa 4 asubuhi.
Wito.
Jamani tuweni makini na maeneo ambayo hatutakiwi kufika".
MWISHO.
Mpenzi msomaji, na hapa ndio mwisho wa kisa hiki cha jamaa yetu kilichomtokea huko jijini DAR mwaka 2015.
Kama nawe una kisa chochote unawe ukashea nasi kwa kutupigia simu kwa mawaailiano yetu yaliyoko chini kabisa ya blog hii iliyoandikwa "contact"
ninani huyu duuu
ReplyDelete