"Na mwenye kupuuza utajo wetu basi atakuwa na maisha ya dhiki"....
Huenda uliikosa sehemu ya kwanza basi bofya hapa chini.
MAISHA YA DHIKI KWA MWENYE KUMSAHAU ALLAAH (1)
_______________________
Baada ya kusoma sehemu ya kwanza sasa unaweza kuendelea na sehemu ya pili ambayo tutazungumzia kisa cha bwana Hemedi Ally kama ifuatavyo.
Anasema;-
"Naitwa Hemedi, nilizaliwa miaka 33 iliyopita katika wilaya ya Handeni mkoani Tanga.
Leo ningependa nishee historia yangu kwa ufupi ili watu huenda wakajifunza japo kidogo. Mada hii inaendana na maudhui ya aya hiyo hapo juu"
Wakati nakua kuanzia umri wa miaka 15 mpaka 23 nakumbuka nilikuwa kijana mwema sana. Sikuwa naacha swala na kusoma Quran. Masaa 24 nilikuwa karibu na Mwenyezimungu. Kwakweli nilikuwa na amani sana katika Moyo wangu na nilikuwa na maisha mazuri sana ingawa sikuwa nimeajiriwa.
Nilikuwa sio mtu wa wanawake, pombe, sigara, matusi wala mambo yote ya maasi. Uso wangu ulikuwa na nuru sana na kila mtu alinipenda na kuniheshimu. Sikuwa nimeoa lakini wazee wote walinipenda na kuniusia katika kheri.
Kuanza umri wa miaka 24
Nilikuwa na rafiki yangu ambaye tulikuwa tukishirikiana wote katika dini lakini ilikuja kutokea yeye alianza tabia chafu za kufanya zinaa. Alinishawishi nami nijaribu nione ladha yake.
Hapa nilianza kupotea kidogo kidogo baada ya kuanza mambo ya wanawake na kibaya zaidi ni kuanza mambo ya uvutaji wa sigara.
Pole pole nilianza kupotea kutoka katika misingi ya dini na kuanza kujikita katika mambo ya dunia. Niliona raha sana kuishi maisha yale na kuona kuwa kumbe nilikuwa nakosa raha ya dunia hapo nyuma.
Mambo yalianza kuyumba
Nilipokuwa na miaka 30 kwa wakati huo nilikuwa nimeajiriwa katika moja ya Kampuni kubwa hapa nchini. Niliachana kabisa na mambo ya dini na kujua maisha yangu.
Tukio ambalo sitolisahau ni baada ya kumtia ujauzito mwanafunzi wa kidato cha tatu katika moja ya shule zilizopo Jijini Dar es salaam ambapo nilikuwa naishi kwa wakati huo. Suala lile lilinifanya kukimbia mji kwa kuogopa kufungwa jela hasa ukizingatia mtoto huyo alikuwa ni wa mwalimu wa shule mojawapo ya Msingi iliyokuwa karibu na mtaa wetu.
Nililazimika kukimbilia mkoa mwingine na kuanza maisha mapya kwa shida sana. Ikumbukwe wakati huo nilikuwa tayari najihusisha na uvutaji rasmi wa bangi na pombe kidogo.
Maisha yalikuwa magumu sana na kuikumbuka hali yangu nilipokuwa mchamungu wakati ule. Niliwaza maisha yale zaidi baada ya kukamatwa na polisi tukivuta bangi na kukaa rumande kwa siku tatu. Hii ilikuwa ni mara ya kwanza kukaa polisi.
Katika maisha haya nilipitia mengi sana ambayo yalinifanya kumkumbuka Mwenyezimungu ambaye nilikuwa nimemuacha kwa muda mrefu.
Kwa sasa nimefanikiwa kuacha Bangi na pombe, lakini bado sijafanikiwa kurudi katika ibada zangu kama zamani.
Ama kuhusu binti ambaye nilimpa ujauzito akiwa kidato cha tatu, nilipata taarifa kuwa alifariki yeye pamoja na mtoto wakati anajifungua. Iliniuma sana na nilijilaumu sana na kuililia nafsi yangu".
Kwa leo naomba niishie hapa. Ila kwa sasa nimeoa na nina mtoto mmoja. Hii ndio stori ya maisha ya bwana Hemedi.
WITO WANGU
Haya ndio maisha ya dhiki kwa mwenye kumuacha Mwenyezimungu na kuamua kuitafuta dunia. Nadhani nawe unaweza kuwa shahidi katika hili huenda umeshapita katika mambo yanayofanana na hayo.
Hustoria ya Hemedi ni ndefu lakini tumeona tuandike kwa ufupi ili nisiwachoshe wasomaji wangu.
Tujitahidi kushika mafundisho ya Mungu, Misingi ya dini, Kisha tutafute riziki ya Halali bila kuvunjua amri za Mungu. Tutapata amani ya maisha ya hapa duniani na kesho Akhera.
Tunaomba msaada kutoka kwa Allaah

Lakini unaweza kupitia makala hizi kujifunza zaidi
Asante sana.
COMMENTS